MJUE MSANII MR. NICE WAKATI HUO.
Kama wewe ni mfuasi na mfuatiliaji sana wa muziki wa kizazi kipya tangu awali basi huwezi kuwa mgeni wa jina la Msanii Lucas Mkenda a.k.a Mr Nice msanii ambaye alitamba na kufanya vizuri sana miaka ya 2000 hadi 2004. Mr Nice alikuwa ni moja kati ya wasanii waliofanya vizuri sana wakati ule na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutangaza taifa la Tanzania hasa kwa miondoko yake ya TAKEU style ambayo iliwateka wakazi wengi sana wa Afrika ya Mashariki.
Mkali huyo wa nyimbo kama King'asti, Fagilia, Kikulacho na Kidalipo alikuwa ni msanii wa kwanza kutoka Afrika Mashariki ambaye aliwahi kufanya tamasha kubwa la muziki nchini Marekani na kuweza kujaza watu wengi zaidi rekodi ambayo ilivunjwa na msanii Diamond alipofanya tamasha la muziki mwaka jana huko Marekani na kuweza kujaza zaidi ya watu 1000 kwenye shoo yake. Kwa mujibu wa Mr Nice anasema kupotea kwake kwenye tasnia ya muziki wa kizazi kipya kulitokana na yeye kupenda starehe kuliko kazi na kupenda sifa kwa watu yaani kutumia pesa kuliko kawaida kitendo kilichosababisha asiwe makini kwenye kazi yake.
Mr Nice amejaribu kufanya juhudi nyingi ili aweze kurejea kwenye tasnia yake ikiwa ni pamoja na hata kujaribu kufanya nyimbo za injili lakini bado mapokezi yake sio makubwa na hajafanikiwa kwa kiasi chake kukonga nyoyo za mashabiki wake kama ilivyokuwa zamani. Kuna wakati Mr Nice alihamia nchini Kenya ili kufanya shughuli za muziki na alikuwa chini ya lebo ya Grandpa lakini kidogo mambo yalienda ndivyo sivyo na kupelekea kuvunjika kwa mkataba wake.
Mwaka 2016 Mr Nice alikuja na wimbo wake wa Kioo ambao pia haukufanya vizuri sana kwenye jamii. Tumkumbuke Mr Nice kwa mengi na wapenzi wengi wa muziki wanatamani kusikia ujio wake mpya na kuona akifanya vizuri kwenye tasnia ya muziki wa kizazi kipya.
Msanii Mr. Nice


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni