MWENGE WA UHURU WIZI MTUPU.

MWENGE wa uhuru umezinduliwa hivi karibuni na Samia Suluhu, Makamu wa Rais katika viwanja vya Jamhuri Mkoani Morogoro. Mwenge huo “utakimbizwa” nchi nzima.
Mwenge huo kwetu utapita, kwenu umepita au bado? Kama bado basi unakuja. Bahati mbaya tu kwamba kwa mara ya kwanza tangu niwe na akili timamu nilihudhuria mbio za Mwenge mwaka 2011 kwetu Singida.
Niliyoyaona yalinifanya niwalaumu watu wote wakubwa kuliko mimi, ambao kila siku wamevumilia mambo ya hovyo yanayofanywa kwa kivuli cha mbio za Mwenge wa Uhuru.
Ilikuwa ni bahati ya pekee kwa viongozi wa serikali kushindwa kufikiri, hadi wakaamua kunialika nihudhurie katika mbio za Mwenge wa Uhuru. Huko nilijifunza mengi.
Watakaokasirika kwa kusoma haya, wajue lengo langu limefanikiwa, kwani sikuwa na lengo la kuwafurahisha tangu nilipofikiria kuandika haya kuhusu Mwenge.
Upuuzi huu unaanzia katika gharama za kukimbiza Mwenge. Msafara huu unahusisha mkuu wa mkoa, wilaya na sekretarieti zote, usalama wa taifa, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), Uhamiaji, Polisi, Jeshi, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi.
Katika hiyo orodha ndefu, watu wote wanalipwa pesa, tangu mkubwa mpaka mdogo, hadi waandishi wa habari. Pesa inayotumika kwa shughuli ya Mwenge ni nyingi. Msafara wa Mwenge unahusisha magari mengi, yanayojazwa mafuta. Magari mengi yenye namba za PT, STK, STL, STJ, RC na magari ya mwenyekiti na katibu wa CCM, pia yapo mengine yenye namba binafsi.
Nikiwa katika Shule ya Msingi Lusilile, ambako yalifanyika mabidhiano kati ya Mkoa wa Singida na Dodoma, niliona takribani magari 120 au zaidi, kwa misafara yote miwili iliyokutana hapo.
Kimsingi, Mwenge unatumia gharama kubwa mno, kiasi kwamba fedha hizo zingetumika kufanya shughuli za maendeleo, baadhi ya kero kwa wananchi ama zingekwisha au kupungua kwa kiasi kikubwa.
Inashangaza kuona kuwa Mwenge ule ulikabidhiwa katika eneo la shule ambayo haikuwa na madawati.
Njia nzima katika Wilaya ya Manyoni, Singida, tangu tumepokea Mwenge, shule zote njiani wanafunzi walikuwa wamejipanga barabarani, hawakusoma siku hiyo. Lakini hata Mwenge haukusimama njiani.
Wananchi wa Lusilile na vijiji jirani waliniambia kuwa kulikuwa na msako maalumu kwa wananchi watakaokiuka kuhudhuria mbio za Mwenge, hivyo walilazimika kujipanga barabarani tangu asubuhi na baadaye kupigwa na jua kali, njaa na kiu zao hadi Mwenge ulipopita.
Wapo waliolazimishwa kucheza ngoma ili ionekane wanaufurahia Mwenge. Kifupi, wapo wananchi ambao hawakufanya kazi za kujiingizia kipato ili kuheshimu amri ya kuhudhuria mbio za Mwenge
Hata hivyo, katika mbio za Mwenge, Mwenyekiti wa CCM na katibu wake, pamoja na viongozi wa Umoja wa vijana wa chama hicho (UVCCM) ni watu wa kuheshimiwa kuliko hata askari wa cheo cha juu.
Kuna bajeti ya kuweka mafuta gari ya Mwenyekiti wa CCM, Katibu wa CCM, wa UWT, na UVCCM, japo wanahadaa kuwa Mwenge ni wa kitaifa. Ni uongo, kuthibitisha hili, huwezi kuona popote risiti ya mafuta kwa magari ya wenyeviti wa mikoa wa TLP, NCCR, CUF, CHADEMA, NLD.
Kichefuchefu kingine ni kwamba kuna fungu la kununua nguo za mapokezi ya Mwenge, zipo tofauti kati ya ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi ya katibu tawala wa mkoa, ofisi ya mkuu wa wilaya Ofisi ya TAKUKURU, ofisi ya Usalama wa Taifa na viongozi wengine.
Pia unakuta kuna sare za mapokezi ya Mwenge zingine za kimbizia Mwenge. Fungu la suti hizo zilitosha kununua madawati kwa ajili ya darasa moja la shule waliyoenda kukabidhiana Mwenge ambayo haikuwa na madawati.
Mwenge unatembezwa na kaulimbiu za “kumulika wezi na wala rushwa,” nilishtuka zaidi tulipokuwa Manyoni Mjini, ukarabati wa mnara wa Mwenge, mnara ambao umejengwa miaka mingi huko nyuma, mnara ulipigwa rangi na kuandikwa kaulimbiu ya “Tumethubutu, tumeweza, na Tunasonga mbele” kwa gharama ya Sh. 2.5 milioni. Haiingii akilini. Watanzania tuache kuhalalisha wizi wa kimachomacho kama huu.
Mwenge ni nini? Kwanini unatumika kama alama katika mavazi na kadi za UVCCM? Mwenge una msafara mrefu kuliko hata msafara wa rais?
Katika msafara